Thursday, April 10 2025

Header Ads

TAKUKURU Yapokonya majengo ya mamilioni TANESA




Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mwanza, imewapokonya waliokuwa watumishi wa shirika lililokuwa linajishughulisha na kupambana, kuzuia, kutibu na kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi nchini (TANESA) majengo manne yenye gharama ya kiasi cha shilingi milioni 420.

Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza, Emmanuel Stenga amesema kuwa majengo hayo yalijengwa na Serikali ya Uholanzi  katika  kiwanja namba 32 kitalu ‘W’ eneo la Kapripoint jijini  Mwanza  na kuanza mchakato wa kuyakabidhi serikalini.

Stenga amesema mradi huo ulikuwa ukitekelezwa kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania na Uholanzi ambapo baada ya mkataba kuisha mwaka 2012, Serikali ya Uholanzi ilitoa maelekezo ya mgawanyo  wa mali zilizokuwa zikitumika katika mradi huo zikiwamo magari na  nyumba.

“Serikali ya Uholanzi iliekeza magari yachukuliwe na wafanyakazi lakini majengo manne yalipaswa kukabidhiwa serikali ya Tanzania, sasa baada ya wenye mradi kuondoka baadhi ya wafanyakazi wa Tanesa  walifanya mchakato wa kinyemela na kujimilikisha na kuanza kupangisha watu na fedha zote zilikwenda mfukoni mwao," amesema.

Kamanda huyo amesema nyumba hizo zilikuwa zikimilikiwa kinyemela na mapato yake yalikuwa yakiwanufaisha watu wachache, hivyo tayari  hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi yao.

Aidha amesema kuwa TAKUKURU wanafuatilia taratibu za kubadilisha umiliki kutoka kwa waliokuwa watumishi wa Tanesa  na kuwa mali ya Serikali ya Tanzania, ikiwemo kurudisha fedha walizopata kupitia nyumba hizo.

No comments:

Theme images by luoman. Powered by Blogger.